Monday, March 10, 2014

KAMA KUNA MTANZANIA ANAISHI KWA TABU BASI NI HUYU JAMAA. MWENYEWE AOMBA MSAADA WAKO

Stori : Imelda Mtema, Bagamoyo
WANASEMA ukistaajabu ya Musa utayaona ya
Firauni, ni kweli ! Ngaweje Said (39 ), mkazi wa
Kijiji cha Zinga, Bagamoyo , Pwani anateseka
na gonjwa asilolijua ambapo nyama kubwa
imeota toka juu ya uso upande wa kushoto na
kumwagikia kifuani , Uwazi lilikutana naye uso
kwa uso.
Akizungumza na mwandishi wetu akiwa
nyumbani kwake kijijini hapo juzi , Ngaweje
alisema:
“ Ugonjwa huu ulinianza nilipozaliwa tu mwaka
1975 pale Hospitali ya Bagamoyo . Kilianza
kipele, lakini kadiri nilivyokuwa nikikua, kipele
nacho kilikua.
“ Sikujua kama itafikia hali hii . Hata wazazi
wangu nao hawakujua , waliamini baada ya tiba
kipele kitanywea , lakini wapi!
“ Baadhi ya watu walishauri nipelekwe Hospitali
ya Muhimbili ambako kuna madaktari bingwa.
Kweli, mwaka 1979 , baba alinipeleka
Muhimbili ambako nilipata tiba na kurudi
nyumbani lakini kipele kilizidi kukua .
“ Mwaka 1995 , mimi mwenyewe nilirudi tena
Muhimbili. Safari hii madaktari waliniambia
watanifanyia upasuaji kwa awamu.
“ Walinifanyia upasuaji , wakaniruhusu kurudi
nyumbani ili nikatafute fedha halafu nirudi tena
lakini hawakuniambia ni shilingi ngapi na pia
sikupata hiyo pesa !
“ Mwaka 2001 sasa ikiwa si kipele tena bali ni
linyama likubwa , niliamua kwenda Hospitali ya
CCBRT, (Msasani, Dar). Pale pia wakaniambia
nikatafute pesa halafu nirudi wanifanyie
upasuaji.
“ Sikuwa na fedha kwa sababu sikuwa na kazi
yoyote ya maana , ni kama nilivyo sasa.
Kuanzia hapo niliamua kuachana na hospitali
nikimtegemea Mungu atakavyoamua .
“ Mbaya zaidi wazazi wangu walishafariki
dunia. Alianza baba , akaja mama kwa hiyo
nikawa sina msaada wowote ule .
“ Nilipanga kuoa nikiamini kwamba mke
atanisaidia , lakini wanawake wananikataa kwa
hali yangu . Na ukiangalia ni kweli , mke gani
atakuwa tayari kuishi na mume mwenye
linyama kama hili , tena usoni?
“ Kwa sasa nahangaika tu, nafanya biashara ya
kuchajisha simu za watu kwa shilingi 200
kwenye chumba nilichopewa . Kwa siku
wanaweza kuja wateja wanne ambapo napata
shilingi 800 tu , hainisadii chochote.
“ Kusema ukweli jamani mimi nakufa, lakini
kama Watanzania wenzangu mpo na
mtaguswa na gonjwa langu hili naombeni
mniokoe. Kuna watu wanasema nikienda India
wanaweza kunifanyia upasuaji nikawa kama
binadamu wengine, lakini nitaendaje huko
wakati sina fedha ?”
Simulizi ya Ngaweje inaumiza sana , hata
mazingira anayoishi si ya kuridhisha. Anasema
anahisi kichwani ana mzigo mzito kutokana na
nyama hiyo kumwelemea .
Anasema: “ Hata nikitembea nahisi kuzidiwa
upande mmoja . Nafsi yangu imekuwa
ikijitenga na watu kwa sababu naamini siko
kamili na pia nahisi nawakera wanaponiona. ”
Ngaweje anahitaji shilingi 5, 000 ,000 ili
kufanyiwa upasuaji nje ya nchi . Kwa wale
watakaokuwa tayari kumsaidia kwa njia moja
au nyingine , wanaweza kuwasiliana naye kwa
namba yake ya simu ya mkononi (Tigopesa )
0659764461.
Kuwasaidia wenye shida ni sehemu ya Ibada
kwa imani zote za dini, ndugu yangu jichotee
baraka kwa kumsadia ndugu yetu huyu
ambaye kiukweli yupo kwenye mateso mazito.

No comments:

Post a Comment

 
Support : KARIBU TENA HABARI YA MJINI
Copyright © 2011. AROUND THE WORLD - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA HABARI YA MJINI
Proudly powered by Blogger