Monday, March 10, 2014

HATARI DAR...FOLENI ZA MAGARI ZASABABISHA MAJANGA MAPYA...!!SOMA ZAIDI HAPA....

Dar es Salaam.
Wakati kukiwa na ongezeko kubwa la
ununuzi wa magari na kusababisha idadi
kubwa ya vyombo hivyo vya usafiri,
foleni za magari nchini, hasa jijini Dar es
Salaam, imefikia hatua ya kutisha huku
ikisababisha madhara makubwa
kiuchumi, kijamii na kiafya, ikiwamo
magonjwa ya akili.
Misululu ya magari ilikuwa ni ya kawaida
kuonekana nyakati za asubuhi na jioni
wakati watu wakielekea na kutoka
kazini, lakini sasa foleni zimekuwa ni za
kawaida katikati ya jiji na maeneo
mengine ambayo ukarabati wa barabara
unaendelea wakati wote.
Wakati kukiwa na kasi ndogo ya
ukarabati wa miundombinu ya usafiri,
kumekuwa na ongezeko kubwa la magari
jijini Dar es Salaam. Pia kumekuwapo na
ongezeko kubwa la idadi ya watu hadi
kufikia milioni 4.3 kwa mujibu wa sensa
ya mwaka 2002 huku vyombo vya usafiri
wa umma (daladala) vikitumia njia zisizo
sahihi (kutanua), kufanya foleni kuwa
kubwa hali inayosababisha jiji kuwa kero
kwa muda wote.
Licha ya jitihada za Serikali kutumia treni
kusafirisha abiria ili kusaidia kupunguza
msongamano wa magari nyakati za
asubuhi na jioni, bado tatizo hilo ni
kubwa. Hivi karibuni Waziri wa Ujenzi,
Dk. John Pombe Magufuri aliagiza
Kampuni ya Strabag, inayojenga
miundombinu ya mabasi yaendayo kasi,
kufungua barabara zilizokamilika ili
kupunguza msongamano.
Kutokana na tatizo hilo, wakazi wa Dar
es Salaam na maeneo mengine
yanayoathiriwa na foleni, wamekuwa
wakilazimika ama kusitisha safari au
kuchelewa kazini na kwenye shughuli
nyingine, huku vyombo vya usafiri
vikilazimisha kufanya safari chache na
hivyo wamiliki kupata fedha kidogo
kuliko matarajio yao.
“Madereva wanapata magonjwa ya akili
kutokana na kero za barabarani,” alisema
Dk. Innocent Godman, ambaye ni mmoja
wa wataalamu wa nyanja tofauti
aliyeongea na gazeti hili kuhusu tatizo
hilo.
“Kwanza ni msongo wa mawazo kuhusu
uchumi kutokana na mafuta mengi
kupotea njiani; pili barabara mbovu; tatu
hasira za kuchelewa anakokwenda; na
nne wanakumbana na askari wa usalama
barabarani ambao wanawakamua fedha,”
alisema mtaalamu huyo wa magonjwa ya
akili na mshauri nasaha kuhusu utumiaji
wa madawa ya kulevya.
Tanzania inaelezwa ni nchi inayoongoza
kwa kuwa na msongamano mkubwa wa
magari katika nchi zilizo Kusini mwa
Jangwa la Sahara.
Zatafuna mabilioni ya shilingi
Katika utafiti wake, Wakala wa Mradi wa
Mabasi ya Kasi (DART), Jumbe Katala
amebaini kuwa foleni husababisha ajali
za barabarani, upotevu wa nishati
(mafuta) na muda wa kukaa barabarani
mambo ambayo husababisha hasara ya
zaidi ya Sh655 bilioni kwa mwaka.
Katika utafiti huo, Katala alibaini kuwa
foleni hizo husababisha kudorora kwa
uchumi, huku bei ya mafuta ipanda
kutokana na mahitaji ya nishati hiyo
kuongezeka.
Alisema kuendesha na kuzima gari mara
kwa mara kwa sababu ya foleni
huongeza matumizi makubwa ya gari na
kuongeza kasi ya uchakavu wake, hivyo
kusababisha gharama kubwa za
matengenezo ya mara kwa mara.
Madhara kiafya
Kiafya, foleni pia zinatajwa kusababisha
maradhi lukuki yakiwamo magonjwa ya
akili, pumu, maradhi ya mfumo wa
hewa, mzio utokanao na mafuta na
maradhi ya moyo.
Msongamano wa magari pia husababisha
wasafiri hasa madereva kuvuta hewa
chafu itokanayo na mafuta ya magari na
maradhi ya mfumo wa hewa kutokana na
kutovuta hewa safi. Dk. Godman alisema
madereva wengi wa Tanzania wana
magonjwa ya akili kutokana na sababu
mbalimbali, ikiwa ni pamoja na foleni.
“Madereva wanapata zaidi ya magonjwa
ya akili hata mara mia moja zaidi,”
alisema Dk. Godman. Dk. Godman
alisema msongo wa mawazo unaotokana
na adha za usafiri nchini umewaathiri
watu wengi na kusababisha wawe na
lugha chafu, hasira za mara kwa mara na
uongo. “Foleni za magari kwa hapa
nchini ni zaidi ya janga kwa sababu
unaathiri kila sekta ya maisha,”
alifafanua.
Kutokana na utafiti huo, madereva wengi
wanaofanya kazi katika maeneo hayo,
hasa katika mabasi ya mijini (daladala)
kwa muda mrefu, wanatajwa kuwa
katika hatari ya kupata maradhi ya akili
kutokana na kuwa na msongo kwa
kipindi kirefu.
“Wengi wao wanavuta bangi, halafu
wakichanganya foleni ya barabarani na
ugumu wa maisha, huo ni ugonjwa wa
akili,” alisema. Wanasayansi wanautaja
ugonjwa huo kwa kitaalamu kuwa ni
‘maradhi ya msongo wa foleni’ (Traffic
Stress Syndrome).
Kuvunja ndoa
Wataalamu wa masuala ya kijamii
wanaeleza kuwa madereva na abiria
wamekuwa wakitumia muda mwingi
kwenye foleni na kusababisha kupoteza
muda ambao wangeutumia kwenye
uzalishaji.
Kutokana na hali hiyo, bila takwimu
wanasema abiria hao wengi hulazimika
kusema uongo kwa kuchelewa katika
mikutano ya kikazi, elimu, biashara na
wakati mwingine watu kuadhibiwa kwa
kuchelewa maofisini na majumbani,
jambo linalosababisha kuyumba kwa
ndoa.
Hasara zaidi
Mhadhiri wa Uchumi, kutoka Chuo Kikuu
cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja
anachanganua hasara ya msongamano
katika mtazamo wa upotevu wa muda na
mafuta.
Anasema, iwapo magari yatachukua
muda mrefu kufika eneo moja, basi hata
bidhaa zitapanda bei, kwa sababu mafuta
mengi yanatumika njiani. “Chombo cha
moto kilichotumia dakika kumi, si sawa
na kilichotumia saa nzima, ukijumlisha
hasara ya mafuta ni sawa na kujenga
barabara zote hapa nchini,”

No comments:

Post a Comment

 
Support : KARIBU TENA HABARI YA MJINI
Copyright © 2011. AROUND THE WORLD - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA HABARI YA MJINI
Proudly powered by Blogger