Saturday, March 8, 2014
MKASA WA ALIYEJIFUNGUA, AKAJIRUSHA GHOROFANI MUHIMBILI NA KUFARIKI DUNIA.
KUNA simulizi ya majonzi nyuma ya kifo cha mwanamke Lewina Kinemo (38) aliyedaiwa kujirusha ghorofani katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dar es Salaam ambako alikwenda kujifungua, Risasi Jumamosi lina mkasa mzima.
Lewina alifariki dunia Jumanne iliyopita saa tano na dakika arobaini alipokuwa anatoka kumnyonyesha mwanaye aliyezaliwa wiki moja nyuma.
MWANAMKE ALIYEKUWA NA MAREHEMU
Kwa mujibu wa mwanamke aliyekuwa na Lewina (jina halikupatikana mara moja) muda mfupi kabla ya kifo, marehemu alifanya mambo yenye viashiria vya kifo chake na hajui nini kilimtokea.
Alisema: “Unajua baada ya kujifungua, watoto waliopatikana na matatizo walitengwa kwenye chumba maalum ghorofa ya pili, sisi wazazi tukawa chini.
“Sasa tulikuwa tunatakiwa kupanda ghorofani kwenda kuwanyonyesha watoto kila baada ya saa tatu kupita. Ili kwenda, ililazimika kupanda lifti lakini kwa sababu yeye alijifungua kwa upasuaji, daktari alimshauri asiwe anapanda lifti.
“Tulipanda mara kadhaa, lakini safari ya mwisho ambayo marehemu alikutana na kifo chake, baada ya kumaliza kumnyonyesha mwanaye, alimshika akamwangalia sana kisha akasema maskini mwanangu sijui utabaki na nani?
“Mimi sikutilia maanani kauli yake, kumbe alijua atakufa.
“Kuna wakati tukiwa wodini alisema yeye ana duka la kushona nguo, akawa anahoji siku atakapokuwa hayupo nani atasimamia biashara zake kwani mumewe naye ni mfanyabiashara kwa hiyo yupo bize.
“Nilimuuliza anataka kwenda wapi hadi anasema hivyo, akajibu amewaza tu. Kumbe mawazo yake ni kama alijua dakika chache mbele ataiaga dunia.
“Sisi tuliokuwa tunatumia lifti tulipofika vyumbani mwetu tulijua yupo nyuma yetu. Kishindo kikubwa cha kitu kizito kuanguka ndicho kilichotushtua lakini hatukutoka nje.
“Baadaye ndiyo tukaletewa habari kwamba mwenzetu mama kichanga alianguka na kufa. Tulishtuka sana, tulilia kwani marehemu alikuwa mchangamfu kwa kila mtu ingawa siku ya kifo kama alipooza au kukosa raha. Kuna mwenzetu mmoja alimuuliza mbona leo huna raha, akasema anawaza maisha yake ya mbele,” alisema mwanamke huyo.
ALIJIRUSHA AU ALIANGUKA?
Mwanamke huyo alipoulizwa kama marehemu alijirusha mwenyewe, alirushwa au alianguka kwa bahati mbaya, alijibu:
“Hatujui. Hata manesi wenyewe walisema walimkuta amekufa chini, kwa hiyo hawajui kama alianguka au alijirusha kwa kuwa hakuna aliyemuona.”
MUME WA MAREHEMU NAYE
Akizungumza kwa uchungu kwenye msiba wa mkewe, Sinza - Mori jijini Dar, mume wa marehemu Lewina aitwaye Mashaka Mkude alisema:
“Kifo cha mke wangu mimi najua kilitokana na uchovu wa kupanda na kushuka kutoka ghorofa ya kwanza hadi ya pili kwa ajili ya kumnyonyesha mtoto.
“Mke wangu akiwa mjamzito alifika Muhimbili akiwa mzima wa afya, akajifungua mtoto wa kike kwa njia ya upasuaji.
“Baada ya kujifungua, hali ya kichanga ikiwa si nzuri kiafya, alionekana ana manjano, yaani hali ya kubadilikabadilika na akalazimika kutengwa yeye na mtoto wake.
“Kutokana na hali hiyo mke wangu alishauriwa na daktari awe anakwenda kumnyonyesha mtoto kila baada ya saa tatu.
“Ilikuwa usiku wa saa sita kasoro, siku ya Jumanne, yeye na wenzake walipoamka kwenda kunyonyesha inadaiwa hakupanda lifti kama wenzake.
“Wakati wa kurudi inadaiwa kuwa marehemu alikuwa na mwenzake wakati wa kushuka, akashauriwa atumie lifti lakini alikataa.
“Baada ya muda mfupi wenzake walisikia kishindo kikubwa kumbe ni mke wangu alianguka kutoka juu na kufariki dunia palepale.
“Nina imani mke wangu alikuwa katika utaratibu wa kutimiza ushauri wa dakrari wake hali iliyompata ilitokana na uchovu wa kupanda ngazi na kushuka,” alisema mwanaume huyo.
Mashaka alikanusha vikali kuwa mke wake alijirusha na kumsababishia kifo, akisema marehemu hakuwa na tatizo lolote la kifamilia wala kiafya.
AZIKWA, KICHANGA BADO HOSPITALI
Habari zinasema kichanga hicho walichokipa jina la Biligita Mashaka kinaendelea vizuri katika uangalizi maalum hospitalini hapo ambapo kinawaliza wengi kutokana na masaibu yaliyotokea.
Marehemu alizikwa Ijumaa ya wiki iliyopita katika Makaburi ya Kinondoni jijini Dar es Salaam. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amina.
KAMANDA WA POLISI ILALA ATHIBITISHA
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Marietha Komba alithibitisha soma hii: PICHA ZA MSANII LULU NA STAA WA MOVIE NIGERIA ZAWAACHA WABONGO VINYWA WAZI.. kutokea kwa tukio hilo ambapo alisema marehemu alikutwa chini amekufa baada ya kuanguka kutoka kwenye ngazi za ghorofani.
Chanzo:Gumzo la Jiji
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment