AMA kweli duniani kuna mambo kwani dereva na abiria wa basi la Manchester ambalo namba yake haikujulikana mara moja, lililokua likitoka Lindi kwenda jijini Dar es Salaam walijikuta wakiangua vilio baada ya kumuona mwenzao akijichinja hadi kufa kwa kisu ndani ya gari hilo. Kwa mujibu wa chanzo, tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa tisa alasiri, Jumatano wiki iliyopita mara basi hilo lilipofika katika hoteli moja ya Nangulukulu kwa ajili ya kupatia chakula.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na waandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita, baadhi ya abiria walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa mara walipofika katika hoteli hiyo, kila mmoja alitawanyika kwa lengo la kujipatia chakula na baadhi yao walienda maliwatoni akiwemo marehemu huyo.
Walisema kwamba marehemu huyo ambaye jina lake halikupatikana mara moja, wakati wa kushuka hakuonekana na kisu aina ya sime lakini baadaye abiria wachache waliotangulia kwenye gari, walimshuhudia akiwa ameshika sime hiyo mkono pasipokujua aliipata wapi.
“Hata sisi tulishangaa kumuona akiwa karibu na usukani wa dereva huku akizamisha sime tumboni kisha kuichomoa na kujichinja shingoni hadi pale alipokuwa akivuta koromeo na kuning’inia.
“Tulichanaganyikiwa kwani ni kitu ambacho hatukukitarajia na wala hatujawahi kushuhudia tukio kama hilo la mtu kujichinja hadharani, tulibakia kutokwa machozi huku akina mama wakipiga yowe, hakuna mtu aliyethubutu kumsogelea kumuokoa kwani kila mmoja alimuogopa.
“Tulishindwa kupanda basi hilo kwani ni tukio la ajabu pia ndani kwa mbele kulikuwa kumetapakaa damu, ghafla alidondoka chini ndani ya gari, aliomba kalamu na karatasi ili kuandika ujumbe.
“Dereva alichukua kalamu na kipande cha karatasi na kumpa, alianza kuandika huku damu ikimbubujika tumboni na shingoni, hatukujua alichokiandika, aliishiwa nguvu taratibu akadondoka.
“Abiria walimsogelea na kumuinua na walimueleza kuwa atubu kwa Mungu kosa alilolifanya kabla hajafa, alipiga magoti na kuomba, ghafla alidondoka tena.
“Kaka yake ambaye alikuwa akisafiri naye kuelekea Dar es Salaam alichanganyikiwa kwani hakutegemea kuwa mdogo wake angejiua, kwani alisema hana historia ya kuugua ugonjwa wa akili. Polisi walipigiwa simu na walifika kumchukua lakini baada ya muda mfupi akawa amefariki dunia.
“Sisi abiria wengine tuliendelea na safari kuelekea Dar es Salaam ambapo marehemu na kaka yake walibakia huko mkoani Lindi.
“Mara tulipofika Dar es Salaam dereva alitusihi tukae kimya kwa dakika moja na kuomba kutokana na tukio lililotupata, tulifanya hivyo baadaye kila mmoja alitawanyika na kuelekea kwake,” kilisema chanzo kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Lindi, ACP Renatha Mzinga alipoulizwa mwishoni mwa wiki iliyopita kuhusiana na tukio hilo alikiri kutokea.
“Ni kweli tukio hilo lilitokea lakini kwa sasa sina data kwani nipo njiani nikitokea Nairobi, Kenya kikazi kuelekea Lindi, mara nitakapofika huko ofisini ndipo nitapata tukio zima lilivyokuwa,” alisema Kamanda Mzinga.
No comments:
Post a Comment